Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wawekezaji Tumieni Teknolojia za Kisasa kutunza Mazingira


aibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe  ameyashauri 
mashirika na  kampuni  za  ndani na nje  ya nchi yanayotaka kuwekeza nchini kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kutumia teknlojia za kisasa zitakazowezesha utunzaji wa mazingira ili   kuvutia wawekezaji wengine zaidi.

Kigahe ameyasema hayo Septemba 27, 2022, jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa Mradi wa Kanda Maalum ya Kiuchumi ya Mkinga Mkoani Tanga unaotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 3000 katika awamu ya kwanza.

Aidha, amewapongeza wawekezaji hao kwa kuziona fursa zilizopo mkoani Tanga na kisisitiza kuwa Serikali itawaunga mkono kwa kuwezesha uwekezaji huo kuwa na tija kwao na kwa Serikali kwa kuwa Sekta binafsi  ni moja ya sehemu kubwa  katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua

" Serikali inatarajia uwekezaji huu kuwagusa moja kwa moja wananchi wa wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga na Taifa  kwa ujumla kwani hiyo ndio itakuwa njia sahihi ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na hivo kuleta Tija katika uchumi wa Taifa" Amesema Kigahe

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mkinga Special  Economic Zone Bw. Ally Kassim amesema lengo la Mradi huo ni kutekeleza maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha uwekezaji nchini unaongezeka ili kuleta usawa wa kiuchumi katika maeneo yatakayofanyiwa uwekezaji husika.

Aidha, amesema Wawekezaji hao wamethibitisha kuwa hadi sasa jumla ya wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali  ikiwemo Brazil, Misri, Tunisia, Bulgaria, GCC, Ufilipino na India wameonyesha nia ya kuwekeza katika  mradi huo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga  Mhe. Omary Mgumba amesema  wawekezaji hao wamevutuwa na fursa mbalimbali ambazo ni  Bandari, Bomba la mafuta pamoja na Ardhi yenye rutuba  zinazowarahisishia  kuapata malighafi na usafirishaji wa bidhaa na vitendea kazi kutoka ndani na nje ya nchi.