Habari
WAZIRI PROF. MKUMBO: NIA YA SERIKALI NI KUONA VIWANDA NA BIASHARA ZINASIAMAMA VIZURI NA KUSHINDANA KIMATAIFA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewahakikishia Wafanyabiashara na wenye viwanda nchini kuwa nia ya Serikali ni kuona Viwanda na Biashara zinasimama vizuri na zinaweza kushindana kimataifa lakini lengo ni kuwa vizalishe ili serikali nayo ipate kodi.
Prof. Mkumbo ameeleza hayo Agosti 12, 2021 mkoani Arusha wakati alipoambatana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe.Daniel Sillo kutembelea Kiwanda cha Nguo cha A to Z ili kuangalia utekelezaji wa shughuli zake pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
“Niwahakikishie wafanyabiashara wote na wenye viwanda kuwa nia ya serikali ni kuona Viwanda vyetu na Biashara zetu zinasimama vizuri na zinaweza kushindana kimataifa lakini wakati huo huo lengo ni kuwa vizalishe kwa kiasi kikubwa ili Serikali nayo ipate kodi” amaeeleza Prof. Kitila Mkumbo
Prof. Mkumbo amesema kuwa Wizara ina mpango wa kuomba Bunge iridhie Tanzania kujiunga na mkataba wa biashara huru ukanda wa Afrika ambapo viwanda vyetu hapa nchini vinahitaji kujipanga zaidi katika ushindani ndani ya Afrika na dunia kwa ujumla hivyo Tanzania ikisaini mkataba huo utasaidia kufungua masoko katika nchi 54 za Afrika.
Aidha, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kamati ya Bunge ya bajeti ndio kamati yenye mamlaka na jukumu la kuishauri Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu masuala ya kodi ili kodi wanazoziweka ziwe ni Kodi ambazo zinachochea uzalishaji katika viwanda na kuweza kushindana katika soko la ndani ya nchi na ukanda wa Afrika hivyo ziara hiyo ni fursa kubwa kwa kiwanda hicho na viwanda vingine.
Naye, mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya bajeti na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mhe. Daniel Sillo amesema kuwa kwenye Bunge lililopita walipata mwakilishi wa kiwanda kicho kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti akieleza changamoto zinazowakabili ndio maana kamati imechukua hatua ya kufika Arusha ili kujionea kiwanda chenyewe.
Mhe. Daniel Sillo ameendelea kueleza kuwa kiwanda cha A to Z kinafanya kazi kubwa sana wanalipa kodi serikalini takribani shilingi bilioni 17 kwa mwaka na kimeajiri zaidi ya watanzania 8,000 hivyo kamati imejionea uhalisia wa bidhaa wanazozalisha na wameelekeza uongozi wa kiwanda hicho kuandika barua ya kueleza changamoto hizo ili waweze kuzichambua na kutoa ushauri kwa Serikali kuona katika bajeti ijayo ni namna gani serikali itaweza kubadilisha viwango vya kodi.
Awali Meneja masoko wa kiwanda Cha A to Z , Silvester Kazi alisema kuwa changamoto kubwa zaidi inayokabili ni marejesho ya VAT ambayo yamechelewa sana ambapo wameiomba kamati iweze kusaidia fedha hizo ziweze kutoka kwa wakati ili waweze kuwekeza na kuongeza uzalishaji zaidi.
Silvester Kazi ameeleza changamoto nyingine ni ongezeko la kodi kwenye nyuzi za pamba kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 25 ambapo wameiomba serikali kurudisha kwenye kiwango cha awali kwani kuna mikataba ya mauzo ambayo walishaingia na haiwezekani kuongeza Bei ya bidhaa hizo tena, hali inayohatarisha ustawi wa kiwanda kutokana na kutarajia kupata hasara.