Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Wito watolewa kwa wafanyabiashara wa mipakani kutumia mipaka halali


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe amewaasa wafanyabiasha kutumia mipaka halali badala ya kutumia njia za panya kuvusha bidhaa mbalimbali kwenda nchi za jirani.

Mhe. Kigahe ameyasema hayo leo 19 Septemba 2024 alipofanya ziara katika mpaka wa Namanga uliopo Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kwa kuongea na menejimenti ya watumishi katika mpaka huo upande wa Tanzania na wawakilishi wa wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali.

Katika kikao hicho Mhe. Kigahe ametumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi wa Serikali wanafanya kazi katika mpaka huo kuwa waadilifu na kuacha tabia ya kushirikiana na wananchi kuvusha bidhaa kwenda nchi jirani kwa kutumia njia zisizo halali ambazo zinaikosesha Serikali mapato.

Katika hatua nyingine Mhe.Kigahe amewaomba watumishi katika mpaka huo kutoa Elimu endelevu kwa wananchi wa Longido hasa wafanyabiashara katika mpaka wa Namanga ili waweze kupata uelewa wa kutosha ,kuhusu ulipaji kodi utakaowasaidia kutofautisha kati ya kodi na ushuru wa gharama mbalimbali wanazotumia.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Idara ya Ushuru na Bidhaa katika mpaka wa Namanga Bw.Edwine Changwe akisoma taarifa ya utekelezaji wa kituo hicho amesema kwamba,kituo hicho kinashirikiana na Idara mbalimbali za serikali ambazo zinasimamia Biashara ikiwemo TBS na WMA.

Vilevile ameeleza kuwa mikakati na malengo ya kituo hicho ni pamoja na kuboresha uhusiano na ushirikiano na mipaka jirani ya Holili na Tarakea ili kubadilishana uzoefu wa matukio ya kukomesha Biashara za magendo.