Habari
WRRB YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI YA MIAKA MITATU KWA KATIBU MKUU WA BIASHARA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah amepokea taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) ya utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitatu kufuatia kukamilika kwa muda wake wa kisheria wa uongozi.
Hafla ya uwasilishaji wa taarifa hiyo imefanyika katika ukumbi wa Wizara ya Viwanda na Biashara uliopo Mji wa Kiserikali Mtumba, jijini Dodoma Oktoba 27, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara, watendaji wa WRRB na wadau wa sekta ya kilimo.
Aidha, Dkt. Abdallah ameipongeza Bodi hiyo kwa kazi nzuri iliyofanyika katika kusimamia na kuimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala nchini, ikiwa ni matokeo ya uwezeshwaji wa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mfumo huo kupitia sera thabiti na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya masoko na maghala.
Dkt. Abdallah ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi mahiri wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mfumo wa stakabadhi za ghala unakuwa chachu ya kukuza biashara, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usimamizi wa masoko ya mazao.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya WRRB, Bw. Godwin Mkanwa ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Bodi na wadau wa sekta ya kilimo. Ameshukuru Wizara kwa kutoa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote cha uongozi wao na kwa kuendelea kulisaidia Shirika hilo kufanikisha majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu ameipongeza Bodi hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kukuza mfumo wa stakabadhi za ghala na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau. Amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano chanya kati ya Serikali, taasisi za sekta ya kilimo, na wadau binafsi. Aidha, amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uwekezaji mkubwa katika bidhaa za kilimo na kwa kuendelea kuutangaza mfumo wa stakabadhi za ghala ndani na nje ya nchi.
