Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Mkutano wa Tatu wa Majadiliano kati ya Serikali na Sekta na Binafsi DODOMA

MKUTANO WA TATU WA MAJADILIANO NGAZI YA JUU KATI YA SEKTA BINAFSI NA SERIKALI UTAKAOFANYIKA TAREHE 19 JANUARI, 2018, UKUMBI WA HAZINA, DODOMA Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo (2016/17 – 2020/21) wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Ili kufikia malengo ya Mpango huu, Serikali inatambua kwa dhati umuhimu na mchango wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wake. Aidha, mchango na matarajio ya Sekta Binafsi yameainishwa bayana katika mpango huu kwa mfano utafutaji wa mitaji na teknolojia na kushirikiana na Serikali katika kuandaa sera, mipango na kanuni zinazoimarisha mazingira ya biashara nchini ili kukuza uchumi. Aidha, katika vipindi tofauti Sekta Binafsi imekuwa ikieleza kwamba inahitaji ushirikishwaji wa karibu na Serikali katika kushauriana ili kuwa na uelewa mmoja katika kuendeleza jitihada za Serikali ya Awamu ya tano kufikia uchumi wa viwanda. Pamoja na kuwa tayari kuna majukwaa mbalimbali ya mashauriano yanayowakutanisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kama vile Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Vikosi kazi vya kisekta, Mheshimiwa Charles J. P. Mwijage, (Mb.), Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, (Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango waliona umuhimu wa kuitisha kikao cha pamoja cha mashauriano kati ya Serikali na Sekta Binafsi kwa lengo la kupata maoni ya Sekta Binafsi katika kuhakikisha malengo ya nchi na maendeleo ya kiuchumi yanafikiwa kwa haraka. Mkutano wa kwanza ulifanyika tarehe 11 Aprili, 2017, kwenye ukumbi wa Hazina Ndogo, Dodoma ambao ulihudhuriwa na Viongozi wa Serikali, Wabunge na wafanyabiashara zaidi ya 200. Upande wa Serikali uliongozwa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Waziri wa Fedha na Mipango. Upande wa Sekta Binafsi uliongozwa na Dkt. Reginald Mengi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Ndg. Salum Shamte, Makamu Mwenyekiti wa TPSF. Miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ilikuwa ni kuwa na mkutano wa aina hii kila robo mwaka, ambapo taarifa ya utekelezaji wa masuala yaliyokubalika itatolewa. Sekta Binafsi imekiri kuwa utaratibu huu umekuwa na manufaa sana kwani hata mapendekezo kadhaa mazuri yaliyopitishwa kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018 yalijumuisha mapendekezo yaliyotolewa kwenye mkutano huo. Aidha, katika mkutano wa pili uliofanyika tarehe 24 Oktoba, 2017 jijini Dar es Salaam, ilikubalika kuwa mkutano wa tatu ufanyike tarehe 19 Januari, 2018 mjini Dodoma kuanzia saa 3:00 asubuhi. Pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, mkutano huo utahudhuriwa pia na Waheshimiwa Mawaziri kutoka Wizara zifuatazo: 1. Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira); 2. Ofisi ya Waziri Mkuu, (Bunge, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) 3. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; 4. Wizara ya Kilimo; 5. Wizara ya Mifugo na Uvuvi; 6. Wizara ya Nishati; 7. Wizara ya Madini; 8. Wizara ya Maji na Umwagiliaji; 9. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; 10. Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi; na 11. Wizara ya Mambo ya Ndani. Wizara inawakaribisha wafanyabiashara wote katika mkutano huo. Kwa mawasiliano zaidi, wawasiliane na Miriam Mondosha wa TPSF kupitia mmondosha@tpsftz.org au +255685885621 na kwa washiriki wa Serikali wawasiliane na Geoffrey Lugongo kupitia geofrey.lugongo@mit.go.tz au +255679861761. KARIBUNI WOTE TANZANIA SASA TUNAJENGA VIWANDA