Habari
BIDHAA 48 ZARUHUSIWA BILA MASHARTI TUNDUMA
Tanzania na Zambia zimekubaliana rasmi kuingiza bidhaa 48 katika mpango wa urahisishaji biashara (Simplified Trade Regime), uamuzi huo unalenga kuwezesha wafanyabiashara wadogo wanaovuka mpaka wa Tunduma na Nakonde kufanya biashara kwa urahisi, bila kupitia masharti magumu ya kiforodha.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah wakati wa Mkutano wa pamoja wa Utekelezaji wa Mkataba wa Mpango wa Urahisishaji Biashara ( Simplified Trade Regime-STR) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia Disemba 19, 2025 Tunduma, Tanzania.
Zoezi hilo muhimu limefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha pamoja cha forodha katika mpaka (OSBP) Tunduma, likitanguliwa na kikao cha pamoja cha siku tatu cha wataalamukutoka pande zote mbili kilichofanyika kuanzia Disemba 17 hadi 19, 2025, kwa lengo la kuweka misingi madhubuti ya kiufundi na kisheria juu ya utekelezaji wa mpango huo.
Dkt. Hashil ameongeza kuwa, mpango huo ni matokeo ya mkataba uliosainiwa awali, ambapo jumla ya bidhaa 48 zimekubaliwa, hivyo wafanyabiashara wadogo kutoka mataifa hayo mawili wanaweza kuingiza na kutoa bidhaa hizo bila masharti magumu ya kiforodha.
Aidha, hatua hiyo itaongeza kasi ya biashara ndogondogo, kuboresha kipato cha wananchi wa mipakani, na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.
Hatahivyo mfumo huo unatarajia pia kupunguza malalamiko na kero zinazokabili wafanyabiashara wadogo, lakini pia kuongeza mtiririko wa bidhaa, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa pande zote mbili.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali, wakiwem, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dkt. Maduhu Kazi, pamoja na balozi wa Tanzania nchini Zambia,Mhe. Luteni Jenerali Mathiew Mkingule, ambapo kwa upande wa Zambia timu ya viongozi waandamizi na wataalamu iliongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda nchini Zambia, Dkt. Simon Ng'ona.
