Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Taasisi zote nchini zinazofanya kazi ya kumlinda mlaji zatakiwa kufanya kazi kwa weledi.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt.Selemani Jafo(Mb) amezitaka taasisi zote nchini zinazofanya kazi ya kumlinda mlaji kufanya kazi kwa weledi.

Amebainisha hayo katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya haki za mlaji Duniani iliyobebwa na kauli mbiu isemayo haki na maisha endelevu kwa mlaji huku ikilenga umuhimu wa mienendo bora ya biashara ya maadili, matumizi yenye uwajibikaji na sera zinazolenga uendelevu zinazolinda mlaji na mazingira.

Dkt.Jafo amesema ajenda ya kumlinda mlaji ni jambo la msingi na haki hivyo bidhaa zisipozalishwa kwa ubora na watu wakipata matatizo taasisi hizo zitakuwa zimeshindwa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.

Dkt.Jafo amesema wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa ya shehena haramu hususan ya mafuta ya kula kupita katika bandari bila kujua usalama wake hivyo ameitaka Tume ya Ushindani(FCC) kushirikiana na mamlaka zingine kufuatilia hilo na kudhibiti kwa nia ya kumlinda Mtanzania.

Aidha Waziri Jafo amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa sehemu muhimu ya Jumuiya ya Maendeleo ya Afrika Kusini (SADC), Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (ACFTA) na masoko mengine ya kimataifa hivyo kuna umuhimu wa kumlinda mlaji katika ngazi ya kanda na kimataifa.

Vilevile Dkt. Jafo amesema Maadhimisho hayo yanachagiza upatikanaji wa bidhaa iliyokuwa bora hivyo inachagiza wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kushindana kuzalisha bidhaa bora zitakayomfanya mnunuzi aweze kuridhika nayo na kulinda usalama wa taifa na kuwahimiza watumiaji wa mwisho wa bidhaa na huduma kutoa taarifa au malalamiko endapo watakutana na changamoto sokoni.

Mwenyekiti wa FCC, Dk. Aggrey Mlimuka, alithibitisha kuwa tume hiyo imekubaliwa kimataifa kwa huduma bora kwa wateja, baada ya kupata cheti cha ithibati yaani ISO 9001:2015 Desemba 20, mwaka jana.