Habari
BALOZI MAHMOUD AIPONGEZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA MAONESHO YA EXPO 2025 OSAKA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb), ameipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa jitihada za kuendelea kutangaza bidhaa za Tanzania kimataifa.
Pongezi hizo zimetolewa Agosti 24, 2025 kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera baada ya Waziri Mahmoud kutembelea banda la Tanzania katika Maonyesho ya dunia ya Expo 2025 Osaka yanayoendelea nchini Japan.
Aidha, Balozi Mahmoud alipata fursa ya kutembelea mabanda ya Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC ikiwemo Zimbabwe, Zambia, Lesotho, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Msumbiji.
Kupitia maonyesho hayo yanayofanyika kwa kipindi cha miezi sita kuanzia April 13 hadi Oktoba 13 2025 Tanzania imeshapata mikataba Saba ( 7) ya ushirikiano wa kibiashara na kiutendaji kutoka taasisi mbalimbali za Kimataifa na Makampuni yenye thamani ya jumla ya Shilingi za Kitanzania zaidi ya Bilioni 38.
Kwa upande wake Meneja kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Bw. Deo Shayo ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Dkt. Latifa Khamis amesema mpaka sasa programu tano kati ya saba zimeratibiwa kwa mafanikio makubwa na kutaja kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya TANTRADE na Wizara mbalimbali za Kisekta pamoja na taasisi zake.
Bw. Shayo ameongeza kuwa baada ya utekelezaji huo sasa imebaki kuratibu Programu ya Wiki ya Madini itakayofanyika mwezi Septemba na Wiki ya Sayansi na Teknolojia inayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.
Mafanikio yanayopatikana ni kielelezo cha juhudi endelevu za Serikali na wadau wake kuhakikisha bidhaa na fursa za Tanzania zinapata nafasi pana katika soko la dunia, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.