Habari
MAELEKEZO YA RAIS SAMIA ‘TANGA YA VIWANDA’ YATEKELEZWA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema jitihada za Serikali katika kufufua viwanda Mkoani Tanga zimeanza kuzaa matunda, akitolea mfano Kiwanda cha African Hamon ambacho kilikuwa hakifanyi kazi lakini sasa kimeanza kufanya kazi na kuajiri zaidi ya vijana 200 kwa ajira za kudumu, jambo linalosaidia kuongeza ajira.
Waziri Kapinga amebainisha hayo Januari 06, 2026 wakati wa ziara yake ya kuona maendeleo na utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa ziara yake mkoani humo likiwa na Lengo la kurejesha hadhi ya Mkoa wa Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama awali.
Amesisitiza kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha viwanda vyote vilivyolengwa vinaanza kufanya kazi kikamilifu, ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi kupitia bidhaa zinazozalishwa hapa Tanzania ambapo baadhi viwanda ikiwemo kiwanda cha Nondo cha Steel Rolling kimeanza majaribio na Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za mbao cha Ply and Panel ambacho kimeanza ukarabati.
Waziri Kapinga pia amesema Serikali itaweka mwakilishi katika kila kiwanda ili kusaidia kurahisisha utatuzi wa changamoto za wawekezaji na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa haraka.
Aidha, Waziri Kapinga amesema juhudi hizo zinaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda, huku viwanda hivyo vikichangia kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira za uhakika, Mpango huo umeelezwa wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema kilio cha muda mrefu cha mkoa huo kilikuwa ni viwanda, kwani awali vilibaki kama magofu, Sasa wanafurahi kuona viwanda vikifufuliwa na ameahidi kuendelea kufuatilia ili kufungua viwanda vipya kila wilaya.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Tanga Mjini Mhe. Kassim Makuberi, amesema sasa wananchi wa Tanga wanakwenda kunufaika na uwepo wa fursa kutokana na uwepo wa viwanda hivyo na kuwahimiza kuchangamkia fursa hizo.
