Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MHE. KATAMBI AIAGIZA TEMDO KUTENGENEZA VIFAA SAIDIZI KWA WATU WENYE ULEMAVU


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Patrobas Katambi (Mb), ameliagiza Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) kutengeneza vifaa saidizi kwaajili ya watu wenye ulemavu ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo ambavyo zinauzwa kwa gharama kubwa.

Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara TEMDO na kujionea mitambo mbalimbali inayotengenezwa na kuzalishwa katika Shirika hilo Desemba 23, 2025 Jijini Arusha.

Amesisitiza katika kuzingatia suala zima la ajira kwa vijana na bunifu na kubainisha kuwa Serikali kupitia Sera na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itawezesha kubaini vipaji na fursa zilizopo ili kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo viwanda.

Aidha, ameliagiza TEMDO kutoa matokeo chanya kwani imefanya vema katika suala zima la uzalishaji wa vifaa tiba, mitambo ya uzalishaji wa sukari na mafuta ikiwemo ya kuwawezesha wajasirimali kutumia mashine mbalimbali kwaajili ya kuongeza mnyororo wa thamani katika mazao na kusisitiza kuendeleza ujasiri huo ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakua ikiwemo utatuzi wa changamoto za ndani pamoja na kuokoa mazingira.

Mhe. Katambi amesema Serikali itaendelea katanua wigo na fursa za kuibua vipaji kwa vijana ikiwemo makundi jumuishi ili waweze kujikwamua kiuchumi ikiwemo kukopesheka katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Temdo, Profesa, Frederick Kahimba amesema shirika hilo limejipanga katika suala la viwanda ikiwemo kuweka mipango mikakati ya kuhakikisha sekta ya ubunifu inakua zaidi, huku akiishukuru Serikali na Wizara ya Viwanda na Biashara kutoa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amesema kupitia fedha hizo wameweza kubuni na kuunda teknolojia mashine na mitambo inayotarajiwa kuhamasisha uwekezaji kwenye Viwanda vidogo vya kati ili kutoa ujuzi na ajira kwa watanzania wengi huku Serikali ikipunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza kutoka nje ya nchi bidhaa, mashine na mitambo ambayo kwa sasa inatengenezwa na TEMDO.