Habari
BALOZI SALUM ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA UZINDUZI, AIPONGEZA TIMU YA MAANDALIZI
📌Awashukuru watendaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara
📌Maandalizi ya uzinduzi wa sera mbili za maendeleo ya viwanda na ujasiriamali yaimarika
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, amewashukuru wakurugenzi na menejimenti ya wizara hiyo kwa maandalizi mazuri yanayoendelea kuelekea uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na wa Kati (Toleo la 2025).
Balozi Salum ametoa pongezi hizo leo, Novemba 1, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma, wakati wa kukagua maandalizi ya uzinduzi wa sera hizo, akipongeza ushirikiano na juhudi za watendaji wa wizara katika kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa ufanisi.
Katika kuelekea uzinduzi huo, kesho Novemba 2, 2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, anatarajiwa kuzindua maonesho ya wafanyabiashara yatakayofanyika katika ukumbi huo. Maonesho hayo yataambatana na kliniki za biashara na kuendelea hadi Novemba 4, 2026.
Aidha, Novemba 3, 2026, kutafanyika kongamano la wadau wa Viwanda na Biashara, kabla ya uzinduzi rasmi wa sera hizo mbili utakaofanyika Novemba 4, 2026, ambapo Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.
