Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitiasha Bajeti  ya Sh.Bilioni 110.89 ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akijibu hoja za Wabunge Mei 22, 2024 Bungeni Dodoma,amesema kuwa ni hatua kubwa sana kwani bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imeongezeka kwa asilimia 20 ukilinganisha na ya  Mwaka wa fedha uliopita ambayo ilikuwa Sh.Bilioni 92.

Aidha, amesema kodi zinakusanywa kisheria hivyo Wizara haipo tayari kukubaliana na ukwepaji wa kodi au kutorejesha kodi inayokusanywa na wafanyabiashara kwa niaba ya serikali.

“Kwa siku naongea na Kamishna wa TRA zaidi ya mara kumi kwa ajili ya changamoto za wafanyabiashara, kodi zinakusanywa kwa sheria, kama umevunja sheria hatuwezi kukubaliana kwenye eneo hilo. Siku hizi TRA wananipigia simu wanakwenda Kariakoo,”amesema.

Amesema wameanza kuendesha kliniki za biashara Kariakoo ambapo kwenye kliniki hizo wapo maofisa wa TRA na maofisa biashara ili kuhakikisha kodi inalipwa na walipakodi wanasajiliwa.

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe(Mb) akizungumzia kipimo haramu cha Lumbesa, amesema wizara kupitia Wakala wa Vipimo imeshaanza operesheni maalumu katika mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Njombe, Morogoro, Iringa.

Amesema wizara yake kwa kushirikiana na Tamisemi wataanzisha vituo ambapo wakala wa vipimo ataweka mizani na kupima mazao ya wakulima.