Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

CBE YAINGIA KATIKA KUMI BORA KITAIFA KATIKA MAHAFALI YAKE YA 60


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miongozo bora anayoitoa kwa Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo imechangia maendeleo bora katika Wizara yake na Taifa kwa Ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa Mahafali ya 60 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Dodoma Disemba 13, 2025 jijini Dodoma, alipokuwa akiwasilisha Salaam za Wizara ya Viwanda na Biashara.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ambaye ndiye mgeni Rasmi amewatahadharisha wahitimu juu ya uwepo wa ajira chache na kuwashauri wajiandae kwa ajili ya kujiajili kwa kuanzisha biashara na kuajiri watu wengine ili kukizidhi mahitaji ya kila siku.

Mhe. Senyamule ameongeza kuwa Serikali imeshaandaa mazingira mazuri kwa vijana wa kitanzania kujiajiri na kujitengenezea maisha mazuri, na kutaja mazingira hayo kuwa ni pamoja na mikopo kwa ajili ya vijana, miundombinu bora ya barabara, umeme na reli ya kisasa ya SGR na kusisitiza juu ya umuhimu wa kutumia huduma bora ya mawasiliano kama fursa ya kutatua changamoto za kiuchumi.

Hata hivyo, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Edda Lwoga amesema katika jitihada za kuleta mapinduzi katika sekta ya biashara nchini mwaka 2023 Chuo hicho kilianza kutoa programu za masters kwa njia ya mtandao na kubainisha mafanikio yake kuwa chuo hicho kimeshika nafasi ya 8 kati ya Vyuo Vikuu 47 nchini kwa kutoa elimu bora kwa miaka miwili mfululizo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Chuo hicho Prof. Zacharia Mganilwa amewaasa Wahitimu kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu kwa faida ya taasisi watakazofanyia kazi na taifa kwa ujumla pale watakaaminiwa na kupata nafasi ya kutumia ujuzi walioupata kutoka katika chuo hicho.