Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Changamoto za Kibiashara kati ya Tanzania na Zambia kutatuliwa


Tanzania na Zambia zimekubaliana kutatua changamoto 25 za kibiashara zilizopo ifikapo Novemba 30, 2023 ili kuiwezesha sekta binafsi kufanya biashara bila vikwazo vyovyote baina ya nchi hizo.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Ashatu Kijaji na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Zambia Mhe. Chipoka Muhenga wa
Zambia wakiwa pamoja na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposya Kihenzile (Mb.) walipokutana
na kushiriki Mkutano wa Pili wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara baina ya nchi hizo uliofanyika katika Mpaka wa Nakonde, Zambia Novemba 07, 2023.


Kwa upande wa Dkt. Kijaji amesema makubaliano ya kutatua changamoto hizo yanatokana na utekelezaji
wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokutana na Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema katika ziara ya Kitaifa nchini humo Oktoba 23 - 25, 2023 na kukubaliana kuiwezesha Sekta Binafsi kufanya
biashara baina ya nchi hizo.


Aidha, amesema nchi hizo pia zimekubaliana kutatua changamoto hizo kwa haraka na kuhakikisha kuwa kila changamoto inayojitokeza baina ya nchi hizo itatatuliwa ili kuiwezesha sekta binafsi kufanya biashara kwa uhuru ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizo kwa kuwa Sekta Binafsi ni injini ya kukuza uchumi kwa mataifa yote mawili


Naye Waziri Muhenga amesema nchi hizo zimekubaliana kutatua changamoto hizo ili kuiwezesha sekta binafsi kujenga uchumi imara chini
ya misingi iliyowekwa na Waasisi wa nchi hizo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda iliyoziwezesha nchi hizo kuishi kwa amani na utulivu