Habari
TANZANIA NA UTURUKI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA VIWANDA NA BIASHARA
Serikali ya Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na viwanda na Uturuki ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050 ya kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu kupitia mageuzi ya sekta ya viwanda, huku serikali ya Uturuki ikiahidi kuendeleza ushirikiano wa kiufundi, kiteknolojia na ubunifu kwenye sekta hiyo.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, nchini Uturuki, ambapo amefanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda na Teknolojia wa Uturuki, Mehmet Fatih Kacır pamoja na Waziri wa Biashara wa nchi hiyo, Ömer Bolat, kwa lengo la kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki, ambacho kwa sasa kimefikia takribani Dola za Marekani milioni 354 mwaka 2026, huku lengo likiwa ni kufikia Dola za Marekani Bilioni moja.
Mhe. Kapinga ametaja maeneo ya kimkakati ya uwekezaji nchini Tanzania, yakiwemo viwanda vya chuma, dawa na vifaa tiba, chakula, pamoja na kongani za viwanda vya kijani (Green Industrial Parks), akisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya malighafi za kilimo na madini ili kukuza ajira na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizochakatwa badala ya kuuza malighafi ghafi.
Aidha katika mazungumzo na Waziri Kacır yamejikita katika kukuza maendeleo ya viwanda vya kimkakati, kuimarisha matumizi ya teknolojia, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda rafiki kwa mazingira, huku pande zote mbili zikikubaliana kuandaa Mkutano wa Tume ya pamoja ya biashara utakaofanyika nchini Tanzania mwaka 2026 ili kujadili kwa kina fursa za kibiashara na uwekezaji.
Kufuatia mazungumzo hayo, serikali ya Uturuki imeahidi kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Tanzania kupitia ubadilishanaji wa teknolojia, ujuzi na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo ya viwanda.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kapinga amezungumza na Waziri wa Biashara wa Somalia, Gamal Hassan, ambapo wamejadili juu ya umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji ili kunufaika vema na fursa za soko la Afrika Mashariki.
