Habari
Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) kuendelea kutoa elimu kwenye Nyanja mbalimbali
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo(Mb) ameuagiza uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara(CBE) kuendelea kutoa elimu kwenye Nyanja mbalimbali hasa kuwajengea uwezo vijana na watumishi mbalimbali wa Serikali kwa kipindi kifupi.
Ameyasema hayo wakati anazungumza na uongozi wa Chuo hicho alipotembelea kuona shughuli na huduma zinazofanywa na taasisi hiyo Septemba 05,2024 Kampasi kuu Jijini Dar es Salaam.
Dkt.jafo amesema elimu hiyo itasaidia kwani kuna uhitaji mkubwa kwa watumishi kupatiwa maarifa juu ya kutimiza majukumu yao na weredi maofisini na amesema amekuwa akifuatilia program inazotolewa kwa wahudumu wa mabasi na kufanya kada hiyo kuwa kada muhimu na yenye ufanisi ukilinganisha na miaka ya nyuma na kwakufanya hivyo kumesaidia vijana wengi kuingia kwenye soko la ajira kwenye sekta binafsi ya usafirishaji.
Aidha ametoa pongezi kwa hatua hiyo ya uendeshaji wa programu mbalimbali na usimamizi mzuri na uanzishaji wa miradi mbalimbali ikiwemo jengo hilo la ghorofa kumi linalojengwa katika kampasi kuu jijini Dar es salaam.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof.Edda Lwoga amesema chuo hicho kinaendelea na mikakati ya kuanzisha kampasi katika Mikoa mbalimbali nchini ili kuongeza wigo wa utoaji elimu.