Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

BIdhaa bandia si tu zinahujumu uchumi wa nchi, bali pia huhatarisha afya na usalama wa wananchi,


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Dkt. Selemani Jafo(Mb) amewataka wafanyabiashara wote wanaozalisha bidhaa nchini pamoja na waagizaji kutoka nje kuhakikisha wanazingatia sheria ya alama za bidhaa, ili kudhibiti uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa bandia katika soko la Tanzania Bara.

Dkt. Jafo ameyasema hayo Juni 25, 2025 jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani, yaliyoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC).

Dkt. Jafo amesema kuwa bidhaa bandia si tu zinahujumu uchumi wa nchi, bali pia huhatarisha afya na usalama wa wananchi, kupoteza mapato ya Serikali na kukatisha tamaa wabunifu halali wa bidhaa.

Aidha, ameiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kushirikiana na wamiliki wa nembo na vyombo vya uwakilishi wa wafanyabiashara ili kutoa elimu ya kutosha kuhusu sheria hiyo na madhara ya bidhaa bandia.

“Ushirikiano kati ya FCC na taasisi za kitaifa na kimataifa ni muhimu kwa kuboresha mbinu za udhibiti, ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa kutambua bidhaa bandia sokoni,” amesema Dkt Jafo

Dkt.Jafo amesema kuwa udhibiti wa bidhaa bandia si jukumu la serikali peke yake, bali ni wajibu wa kila mdau katika mnyororo wa biashara.
Hata hivyo Dkt.Jafo,amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya kisasa kutambua bidhaa bandia kama matairi ya magari, vyakula, nondo na nguo.

Naye, Mwakilishi wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Pauline Gekul,ametoa wito kwa Serikali kuongeza jitihada za udhibiti wa bidhaa bandia, hasa kwenye sekta za simu na vyakula.

Kadhalika, Mwenyekiti wa Bodi ya FCC, Dk. Aggrey Mlimuka, amesema kuwa lengo la udhibiti wa bidhaa bandia ni kuendeleza mazingira ya biashara na kulinda maslahi ya walaji.

Dkt.Mlimuka amefafnua kuwa FCC inashirikiana na wadau wa Zanzibar kuelimisha kuhusu madhara ya bidhaa bandia, kufanya ukaguzi, na kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema kuwa ofisi zao za kanda zinazohudumia zaidi ya mikoa 16 zimeendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kufanya ukaguzi ili kubaini bidhaa zisizo halali.