Habari
NAIBU WAZIRI KATAMBI: TUMIENI ELIMU MLIYOIPATA KUTATUA CHANGAMOTO ZILIZOPO KWENYE JAMII
Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), amewasisitiza wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kutumia elimu waliyoipata kutatua changamoto zinazozikabili jamii zao.
Ameyasema hayo Disemba 6, 2025 akizungumza wakati akimwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, katika mahafali ya 60 ya CBE na ya 18 kwa Kampasi ya Mwanza, yaliyofanyika chuoni hapo.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ili vijana waweze kuwa sehemu ya suluhisho la maendeleo ya nchi, akisisitiza umuhimu wa wahitimu kuchangamkia fursa zilizopo kwa lengo la kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka.
Kwa upande wakeNaye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt Samia Suluhu Hassan yamepelekea cho hicho kuwa na wahitimu wanaofika elfu sita (6,000) kwa mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mohammed akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wahitimu, wanafunzi pamoja na wazazi kulinda amani ya nchi kwani bila amani wasingeweza kufanya sherehe hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo, Prof. Edda Lwoga, amesema kuwa CBE imeendelea kujitanua katika maeneo mbalimbali nchini kwa kufungua kampasi na kutekeleza maelekezo ya Serikali, ikiwemo agizo la Mhe. Rais la kuanzisha kampasi kwenye mikoa ya kaskazini huku akiweka wazi kuwa hatua hiyo imeanza kutekelezwa kwa kupatikana eneo la ujenzi mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Bodi ya CBE, Prof. Zacharia Mganilwa, akizungumza mbele ya mgeni rasmi, ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964, chuo kimepiga hatua kubwa za maendeleo, ikiwemo kushika nafasi ya 8 kati ya vyuo 47 vya elimu ya juu nchini kwa ubora kwa miaka miwili mfululizo. Aidha, amebainisha ongezeko la wanafunzi kufikia 23,111 katika kampasi zote, ambapo 2,181 wanatoka Kampasi ya Mwanza.
