Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

NAIBU WAZIRI KATAMBI ATATAKA CHUO CHA CBE KUTOA ELIMU YENYE USHINDANI KIMATAIFA


Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kuhakikisha kinatoa elimu yenye viwango na hadhi inayoweza kukidhi ushindani katika soko la dunia.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa elimu inayotolewa inapaswa kuwa na ushindani unaoweza kutatua changamoto za mtu mmoja mmoja, jamii, taifa na ulimwengu kwa ujumla, Desemba 19, 2025.

Aidha, Naibu Waziri amekitaka chuo hicho kuongeza nguvu katika utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, akibainisha kuwa kundi hilo ndilo lenye mzunguko mkubwa wa fedha lakini halijapewa kipaumbele cha kutosha.

Ameeleza kuwa CBE inapaswa kuimarisha tafiti zenye tija zitakazochochea mwamko wa elimu, kubainisha changamoto zilizopo na kutoa suluhu zake na kusisitiza kuwa ushauri unaotolewa na serikali lazima utokane na tafiti za kina ili kufanya maamuzi yasiyopotosha.

Vilevile amesema CBE inaweza kuwa mshauri mzuri kwa taasisi za kifedha, hususan benki zinazotoza riba kubwa kwa wajasiriamali hao ili kusaidia ukuaji wa biashara zao nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga, amesema chuo hicho kimeanza kujitanua kimataifa kwa kuwajengea uwezo wahadhiri wake pamoja na kuanzisha programu mpya za kimataifa.

Naye Afisa Miliki wa chuo hicho Bw. Osward Mtei akizungumzia ujenzi wa jengo la Metrology, amesema mradi huo ulianza Mei 25, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mei 23, 2026 ukigharimu jumla ya Sh. Bilioni 26.47 kwa awamu zote mbili.