Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

NAIBU KATIBU MKUU ASHIRIKI UGAWAJI WA TUZO ZA MASOKO (TMCA) NA TUZO ZA CHAPA BORA AFRIKA 2026


📌 Asisitiza matumizi ya teknolojia, ubunifu na ubora katika kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania kupitia Tuzo za Masoko (TMCA) 2026.

📌 Ahimiza kampuni na wafanyabiashara kujenga chapa zinazoaminika na kuzingatia viwango ili kuongeza thamani ya bidhaa za ndani kupitia Tuzo za Chapa Bora Afrika 2026.

📌 Apongeza TanTrade kwa kuunganisha wazalishaji na wanunuzi na kutangaza bidhaa za Tanzania kupitia chapa ya Made in Tanzania.

📌 Wadau wahimizwa kushirikiana kukuza viwanda, biashara, ajira na upatikanaji wa masoko ya ndani na kimataifa.

DAR ES SALAAM

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Aristides Mbwasi, ameshiriki ugawaji wa tuzo katika Kongamano la Saba la Masoko na Tuzo za Mwaka (Tanzania Marketing Congress and Awards – TMCA 2026) na hafla ya Tuzo za Chapa Bora Afrika (Best Brand Awards Africa 2026), zilizofanyika tarehe 13 Novemba 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. Mbwasi alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla zote mbili na kukabidhi tuzo kwa washindi, akiambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Balozi Mafuru, pamoja na mwanzilishi wa Kongamano la Masoko, Prof. Emmanuel Shao. 

Akizungumza katika Kongamano la Saba la Masoko na Tuzo za Mwaka (TMCA), Mbwasi amewahimiza wataalamu wa masoko, wazalishaji na wafanyabiashara kutumia teknolojia, hususan masoko ya kidijitali, biashara mtandao na akili mnemba (AI), katika kuongeza ushindani wa bidhaa na kuwafikia wateja wengi zaidi. 

Aisha amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, ubunifu, viwango na uelewa wa mahitaji ya soko, akieleza kuwa matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuongeza ufanisi wa biashara na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kwa upande mwingine, Mbwasi ameipongeza TanTrade kwa mchango wake katika kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini na kupanua masoko kwa kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi kupitia chapa ya Made in Tanzania na kuongeza kiwan juhudi hizo ni muhimu katika kujenga utambulisho wa bidhaa za Tanzania na kuongeza imani ya walaji katika masoko ya ndani na kimataifa. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Ephraim Balozi Mafuru, amesema mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi ili kuendeleza upatikanaji wa masoko ya uhakika ya ndani, kikanda na kimataifa.

Katika hafla ya Tuzo za Chapa Bora Afrika 2026 (Best Brand Africa 2026), iliyoanzishwa na Zakayo Shushu, Mbwasi ameshiriki kukabidhi tuzo kwa washindi waliotambuliwa kwa ubora wa chapa zao. Hafla hiyo imekuwa sehemu ya kutambua mchango wa chapa katika biashara na kuhamasisha wadau kuendelea kuboresha bidhaa na huduma zao ili kukidhi mahitaji ya walaji na kuongeza ushindani katika soko.

Akitoa maelekezo katika hafla hiyo, Mbwasi amewahimiza wazalishaji na wafanyabiashara kujenga chapa ya Made in Tanzania inayowakilisha ubora, uaminifu, ubunifu na thamani, huku akisisitiza umuhimu wa kuachana na dhana kwamba bidhaa za nje ni bora kuliko zinazozalishwa nchini na kuwataka wafanyabiashara kusajili biashara na chapa zao, kulinda haki miliki, kuzingatia viwango na kuepuka vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuathiri imani ya walaji.

Pia  amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya kampuni kubwa, viwanda na wajasiriamali wadogo na wa kati, hususan vijana na wanawake, ili kuwawezesha kushiriki katika minyororo ya thamani kupitia ujuzi na teknolojia na kuwapongeza washindi wa tuzo hizo na kuwakumbusha kuwa kutambuliwa kwao ni chachu ya kuendelea kuboresha bidhaa na huduma. Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza viwanda, biashara na ubunifu, kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani, ajira na mauzo ya nje.