Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Dk Kijaji afunga maonyesho ya wiki ya viwanda huku akiwasihi wafanyabiashara nchini kuwa waaminifu na waadilifu wanapouza bidhaa kupitia mtandao.


Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amefunga maonyesho ya wiki ya viwanda huku akiwasihi wafanyabiashara nchini kuwa waaminifu na waadilifu wanapouza bidhaa kupitia mtandao.

Amesema wizara ipo mbioni kukamilisha mkakati wa biashara mtandaoni ambao utawezesha wafanya biashara nchini kuuza bidhaa zao kwa njia ya mtandao kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa mizigo wanayoagiza kutoka kwa wafanyabiashara siyo inayokwenda kupokea mteja.

“Tunauziana bidhaa sasa hatuonani, wewe upo kwako yeye yupo kwake na kumekuwa na malalamiko kadhaa ya bidhaa unayoonyesha kwenye mtandao siyo mteja anayokwenda kuipokea. Biashara ni imani, uadilifu nawaomba muwe hivyo ili tuwahudumie na tusiachwe nyuma na mapinduzi ya nne ya viwanda kuelekea ya tano,” Amesema Dkt.Kijaji.


Katika hatua nyingine, amesema anatamani kuona mchango wa sekta ya viwanda unachangia kwenye uchumi wa viwanda kwa asilimia 20 kwenda juu kwa mujibu wa sera ya viwanda badala ya asilimia iliyopo sasa.

“Pia Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo tunahitimisha mwakani imetueleleza huko, hatuwezi kufika huko kama tutafungiana milango, tutatengeneza ukiritimba wa kuhudumiana, tuendelee kuwahudumia na kutengeneza ajira kwa vijana wa kike na kiume nchini,”amesema. 

Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maono ya kuhakikisha sekta binafsi inakuwa sehemu ya kuchangia uchumi wa nchi.

Amewahakikishia wabunge kuwa ushauri walioutoa kuhusu maonyesho hayo utafanyiwa kazi na mwakani watahakikisha wanaweka bidhaa zote ili yafane zaidi.