Habari
Dkt Kisaluka Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ujenzi wa Kongani ya Viwanda- Kwala Pwani

Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi . Dkt. Moses Kusiluka amesema
Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika ujenzi wa Mradi mkubwa wa Viwanda zaidi ya 200 unaoendelea kutekelezwa katika eneo la Kwala Kibaha Mkoani Pwani.
Balozi Kusiluka ameyasema hayo Januari 5,2024 katika ziara yake ya kutembelea viwanda viwili vya nguo na vipodozi vilivyojengwa ndani ya Kongani ya SINO TAN ,Kwala wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, huku akiwa ameambatana na Waziri wa fedha Mwigulu Nchemba ,Waziri wa Viwanda na Biashara na makatibu wakuu wa wizara ya Uchukuzi,Fedha,Viwanda na Biashara na Taasisi wezeshi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inaunga mkono jitihada zinazofanywa na wawekezaji na itahakikisha
Mradi huo muhimu na wenye faida nyingi hususani katika kuongeza ajira, Pato la Taifa na ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla unakamilika.
Kwa upande wa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amesema Mradi huu unaojumuisha viwanda zaidi ya 200 utakapokamilika utatoa ajira zaidi ya laki moja na vijana wengi kutoka ndani ya Mkoa wa Pwani na Taifa kwa ujumla watapata ajira hali itakayoimarisha uchumi wa Taifa kwa ujumla
"Zaidi ya Asilimia 90 ya mabinti ambao tuliowaona katika kile kiwanda cha kutengeneza nguo wanatoka hapa Kwala na waliniambia kabisa kuwa walitembea mitaani kwetu na kuweza kuwachukua wadada kila aliekuwa na cherehani yake nyumbani na kuanza nao hapa na wengine wanakuja". Amesema Kijaji
Aidha Dkt Kijaji alibainisha kuwa katika ziara hiyo walitembelea viwanda viwili kati ya 200 na kimoja wapo ni cha kutengeneza nguo [vijora] zinatumika ndani ya Tanzania na vinauzwa Dubai ambapo bidhaa hizo zinachangia upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na uwekezaji unaoendelea.
Naye Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba, amesema Wizara ya fedha ni wadau wa kila uzalishaji,hivyo wanaunga mkono juhudi za ujenzi wa kongani hiyo na watashughulikia watashughulikia changamoto zinazogusa wizara hiyo.
Awali mratibu wa mradi wa kongani ya Sinotan Jensen Hung alisema, kongani ya Sinotan ,wanatarajia kujenga viwanda vya kati na vikubwa 300 na kutoa ajira za moja kwa moja 100,000.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakari Kunenge alieleza kuwa Mkoa wake umejipanga vizuri katika suala la uwekezaji na ujenzi wa viwanda.