Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT SERERA ASIFU MIKAKATI KUKUZA MASOKO YA KIMATAIFA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera amepongeza mikakati na jitihada za kutangaza bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Dkt. Serera ameyasema hayo Agosti 23, 2025 alipotembelea maonyesho ya Expo 2025 Osaka, Japan ambayo kwa Tanzania yanasimamiwa na Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na kushuhudia bidhaa za kipekee na fursa za utalii na uwekezaji kutoka Tanzania zikitangazwa katika uga wa kimataifa.

Bidhaa hizo ni pamoja na madini mbalimbali kama vile Tanzanite, Dhahabu; mazao mbalimbali ya kilimo kama kahawa, chai, karafuu pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii kukiwa na lengo la kukuza utalii na uwekezaji kwa kutangaza fursa mbali mbali za uwekezaji na utalii zilizopo Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Naibu Katibu Mkuu amepata fursa kujionea jinsi Teknolojia Mtandao inavyorahisisha biashara katika Minada mbalimbali ya Mitambo ya mizigo na magari nchini Japani.

Naye Bw. Deo Shayo ambaye ni Meneja kutoka TANTRADE aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Dkt. Latifa Khamis amesema katika maonesho hayo yanayofanyika kuanzia April 13 hadi Oktoba 13, 2025 Tanzania imeshanufaika kwa kupata mikataba saba (7), ya ushirikiano wa Kibiashara na kiutendaji na taasisi mbalimbali za kimataifa yenye thamani ya shilingi bilioni 38.

Akizungumzia mafanikio hayo Bw. Deo Shayo, amesema tayari programu tano (5) zimesharatibiwa kwa mafanikio na TANTRADE katika maonyesho hayo ya kimataifa kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika.

Hata hivyo, amesema kuwa programu mbili pekee ndizo zilizobaki kufanyika, ambazo ni Wiki ya Madini itakayofanyika mwezi Septemba na Wiki ya Sayansi na Teknolojia mwezi Oktoba.