Habari
DODOMA KUWA KITOVU CHA UTALII WA NDANI, VIJANA WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Dkt.Selemani Jafo amesema Mkoa Dodoma sasa unakwenda kuwa kitovu cha utalii wa ndani Nchini kwa kuzingatia vivutio lukuki na fursa ambazo serikali imezitengeneza Mkoani humo hivyo vijana ni muda muafaka wa kutumia fursa hiyo kwa kwani ni nguzo muhimu katika sekta ya utalii.
Amebainisha hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Majaliwa Kasim wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Mkakati wa Utalii Mkoa wa Dodoma August 21,2025 Jijini Dodoma.
Dkt.Jafo amesema vijana wanapaswa kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kitalii kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Dodoma unakua katika sekta zote huku ukiwa na vivutio ambavyo vinaweza kuwaletea vipato vijana.
Waziri Jafo ameongeza kuwa vijana wanaweza kuhimili mikiki ya mabadiliko ya kibiashara na kuongeza mapinduzi ya utalii Mkoani humo na kuongeza kuwa serikali inatazama kuanzisha Kijiji cha utalii Mkoani humo.
Aidha Waziri Jafo amesema uanzishwaji wa Kijiji cha utalii Mkoani Dodoma utaleta fursa za ajira, biashara na mafunzo kwa vijana huku kikihifadhi urithi wa kihistoria Mkoani Dodoma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema wazo la kufanya Dodoma kuwa kitovu cha utalii wa ndani limekuja wakati muafaka kwani Dodoma inavivutio vingi, ukiachilia kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi, Dodoma ni mkoa pekee unaozalisha Zabibu Nchini hivyo kufanya kuwa mkoa pekee unaotengeneza mvinyo Asili ,juice, na mchuzi wa Zabibu.
Rosemary Senyamule amesema mkoa wa Dodoma ni mkoa pekee wenye makao makuu ya vitu vingi ikiwemo, jengo zuri na la pekee kubwa Africa la Mahakama kuu( Judicial square), Bunge, Ikulu nzuri na ya kipekee, pamoja na uwanja wa ndege wa kimataifa unaotarajia kukamilika, Barabara ya mzunguko pamoja na station ya SGR ya Dk Samia Suluhu Hassan.