Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT. HASHIL AIAGIZA TBS KUTUMIA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 KAMA FURSA YA KUTANGAZA HUDUMA ZAKE


Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hashil Abdallah ameuagiza uongozi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutumia maadhimisho ya Miaka 50 kama fursa ya kutangaza uwezo na huduma zinazotolewa na Sihirika hilo.

Dkt.Abdallah amebainisha hayo Septemba 18,2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa maadhimisho hayo ya Miaka 50 ya Shirika hilo ambapo kilele chake ni kitakuwa mwezi desemba 2025.

Dkt.Abdallah amesema kuwa kwa kutumia fursa hiyo kutafikia lengo la maadhimisho kama kaulimbiu inavyosema“Uhamasishaji Ubora na Usalama kwa Maisha Bora”ambayo itasaidia kuendelea kujenga uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa uzingatiwaji wa viwango vya ubora na uimarishaji soko la bidhaa na huduma zinazokidhi viwango.

Aidha amesema Katika kipindi chote cha miongo mitano, TBS imepiga hatua kubwa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kutanua wigo wa utoaji huduma na kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi na wadau kutokana na kuboreshwa kwa mifumo ya kielektroniki na uimarishaji wa ofisi za kanda pamoja na ujenzi wa Maabara mpya na za kisasa Jijini Dodoma, Mwanza na kukamilika kwa usanifu wa Mradi wa ujenzi wa Maabara jijini Arusha.

Vilevile Dkt.Abdallah ameongeza kuwa katika kipindi cha Miaka 50 TBS imejenga heshima kubwa Kimataifa kutokana na utekelezaji mahiri wa majukumu yake kwa kupata tuzo mbalimbali ikiwemo Tuzo ya Mdhibiti Bora Barani Afrika na kupata daraja la juu la WHO, kuwa wa kwanza SADC kupata ithibati ya kimataifa ya uthibitishaji ubora, na ilifanikiwa kupata ithibati ya kimataifa ya mfumo wa usimamizi wa chakula.

Katibu Mkuu huyo amewaomba wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, wajasiriamali, wanahabari na wadau wengine wote kuunga mkono maadhimisho hayo ili kufanikisha kwa ufanisi kwani TBS ni Shirika la wote na wadau wote ni sehemu ya maadhimisho hayo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt.Ashura Katunzi amesema maadhimisho hayo yatakuwa na matukio kama Viwango Marathon na Viwango Business Forum na sherehe za kilele cha maadhimisho hayo ambayo yatawakutanisha wadau zaidi ya mia tano (500) wa masuala ya ubora, viwango, viwanda na biashara kutoka ndani na nje ya nchi, Uzinduzi wa Kitabu cha historia ya TBS na Maonesho ya Biashara.