Habari
Dkt. Jafo : Serikali itaendelea kulinda Biashara za Wazawa
Dkt. Jafo : Serikali itaendelea kulinda Biashara za Wazawa
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo(Mb), amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kupeleka hati ya dharura bungeni ili kuwezesha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyolenga kulinda biashara za wazawa kuingizwa kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) wa mwaka huu.
Dkt. Jafo amesema hayo Juni 6, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akipokea Taarifa ya Timu maalum ya Ukaguzi wa Biashara zinazomilikiwa na wageni. Katika Soko la Kariakoo.
Aidha, amesema Serikali itahihikisha mapendekezo ya Timu hiyo yanafanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa fursa za kiuchumi na kibiashara zinazalishwa na kusalia mikononi mwa Watanzania.
Amesema tayari timu hiyo imekamilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali, na kwamba wafanyabiashara nchini walishirikishwa kikamilifu kutoa maoni ambapo baadhi ya mapendekezo hayo ni pamoja na kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usajili wa Kampuni, Sura ya 212 ya mwaka 2002, Sheria ya Leseni no 25 ya 1972 na Sheria ya Uhamiaji sura ya 54 na marekebisho ya mwaka 2026 pamoja na Sheria ya Uwekezaji ambazo kwa sasa zimekuwa zikitumiwa kama mianya ya kuingiza wageni kwenye maeneo yaliotengwa kwa wazawa.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya kazi ya kisheria kwa mujibu wa mapendekezo ya Timu na kwamba kama Haru ya dharura itapata kibali, vifungu hivyo vitaingizwa moja kwa moja kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka huu.
Hata hivyo Dkt.Jafo amesema iwapo hati hiyo haitapata kibali, Serikali itahakikisha vifungu hivyo vinapelekwa kama mswada maalum au vinajadiliwa katika mabunge yajayo ili kupata sheria madhubuti ambayo itaondoa mianya inayotumiwa na baadhi ya watu kujinufaisha kwa njia isiyo halali.
Ameongeza kuwa hatua hii inalenga kulinda biashara zinazofanywa na Watanzania na kuweka msingi imara wa kisheria kwa maendeleo ya muda mrefu.