Habari
DKT.JAFO AAGIZA BODI MPYA YA TANTRADE KUSIMAMIA UWAJIBIKAJI NA UADILIFU.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameiagiza Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kusimamia uadilifu na Uwajibikaji ndani ya Taasisi ili kuleta maendeleo ya taasisi hiyo.
Dkt. Jafo ametoa maagizo hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo Agosti 22, 2025 katika Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es salaam.
Waziri Jafo amesema Bodi hiyo ina wajibu wa kusimamia vizuri rasilimali fedha, kuleta ubunifu mpya, kusimamia uadilifu na uwajibikaji wa watumishi na ushirikiano baina ya bodi na wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Aidha Waziri Jafo ameiagiza Bodi hiyo kuandaa mpango mkakati wa Kufanya Viwanja vya Maonesho Sabasaba Jijini Dar es salaam kuwa kituo muhimu cha Mikutano ya Kimataifa
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewagiza Watumishi wa TanTrade kutoa ushirikiano mkubwa kwa wajumbe wa Bodi hiyo Mpya ili kujenga taasisi yenye umoja na ushirikiano kwa maendeleo zaidi.