Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT.JAFO AAGIZA KUKAMATWA KWA BIDHAA FEKI,ASEMA NI HATARI KWA AJIRA NA AFYA.


DKT.JAFO AAGIZA KUKAMATWA KWA BIDHAA FEKI,ASEMA NI HATARI KWA AJIRA NA AFYA.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Selemani Jafo ameziagiza Tume ya Ushindani (FCC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha wanakomesha kabisa uingizwaji wa bidhaa feki nchini, akisema kuwa vitendo hivyo vinahatarisha viwanda vya ndani, ajira za Watanzania na mapato ya serikali pamoja na afya za Watanzania.

Dkt. Jafo ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake katika kiwanda cha ChemiCotex kilichopo jijini Dar es Salaam, Agosti 13,2025 ambapo alielezwa kuwa moja ya bidhaa za kiwanda hicho ni whitedent ambazo zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya ushindani kutoka kwa bidhaa feki.

Dkt. Jafo amesema viwanda vya ndani visipolindwa watanzania watapoteza ajira ambayo serikali imeipa kipaumbele hivyo kuna haja kunwa ya kulinda kiwanda hicho kwani hiyo ni fahari kubwa sana kwa taifa.

Aidha Waziri Jafo amesema Mtu anayegushi bidhaa za ndani anaua soko la wazalishaji wa ndani, kukosa kodi, kupoteza ajira, na kuua viwanda vya ndani hivyo ni muhimu TBS pia kuhakikisha bidhaa zote zinazouzwa nchini zinakidhi viwango vya ubora, na kwamba biashara ya bidhaa feki inahatarisha pia afya ya wananchi.

Pia Waziri Jafo amesema myu anayevuruga bidhaa za ndani ni adui wa Tanzania hivyo amewataka wafanyabiashara na wazalishaji kutoa elimu kuhusu bidhaa halisi ili kuwasaidia wananchi kutambua bidhaa halisi na bidhaa bandia.

Kwa upande wake Meneja wa Rasilimali Watu wa ChemiCotex, Bi. Veronica Senkoro, alisema kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 1,500, ambapo asilimia 63 ni wanawake na pia ameishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini.

Bi. Senkoro pia amesema Kiwanda hicho kimelipa jumla ya shilingi bilioni 110 kwa kipindi cha miaka mitano kama kodi, na bidhaa zao zinasafirishwa hadi Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki.