Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT SERERA: TANZANIA NI MSHIRIKA ANAYEAMINIKA KATIKA BIASHARA NA UWEKEZAJI


Naibu Katibu Mkuu Wizara wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera amesema Tanzania iko tayari kwa uwekezaji na biashara kama Mshirika anayeaminika kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kutimiza malengo ya kujenga uchumi wa viwanda shindani na kuwa Taifa lenye kipato cha juu ifikapo mwaka 2050.

Ameyasema hayo Agosti 27, 2025 wakati akifungua rasmi Kongamano la tatu la Biashara la Watendaji Wakuu 200 la mwaka 2025 lililofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam

Ameeleza kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inatekeleza hatua kadhaa ikiwemo kuondoa kero kwenye kodi na kurahisisha usajili wa biashara.

Mbali na hilo, amebainisha kwamba Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu mikubwa kama reli ya kisasa (SGR), bandari na nishati, pamoja na Kilinda uwekezaji na kutoa motisha za kifedha katika sekta za kipaumbele kama kilimo na viwanda.

Dkt. Serera pia amesisitiza umuhimu wa sekta ya fedha ni kushirikiana na wazalishaji wa ndani kwa kutoa mikopo nafuu ili kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa,

“ bila mtaji viwanda haviwezi kukua, hali itakayoifanya Tanzania kuendelea kuuza malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani” amefafanua Dkt Serera.

Aidha, ametoa wito kwa sekta binafsi kutumia jukwaa hilo kuwasilisha changamoto zinazokwamisha uwekezaji na kupendekeza sera mpya zitakazovutia mitaji, kwa Serikali.

“Tushirikiane pamoja Serikali, wazalishaji, taasisi za fedha na sekta binafsi ili kujenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda shindani na jumuishi kwa wote.” amesema Dkt. Serera.