Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

DKT. SULEIMAN SERERA ASEMA TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA SEKTA YA HUDUMA KUTOKANA NA ONGEZEKO LA USHIRIKI WA WANANCHI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Hassan Serera, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika eneo la utoaji wa huduma, hasa kutokana na ongezeko la watanzania wanaoshiriki moja kwa moja katika uwekezaji na utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Amebainisha hayo wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyoandaliwa na Taasisi ya CSW Oktoba 08,2025 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Serera amesema maendeleo hayo yanaonesha namna ambavyo nchi imeendelea kuwaandaa wananchi wake kushiriki kikamilifu katika sekta ya huduma na biashara kwasababu kipimo cha kwanza ni aina ya watu wanaohusika katika uwekezaji na Wanaotoa huduma nyingi sasa ni Watanzania wazawa, jambo linaloonesha kuna hatua kubwa katika kuwaandaa watu wetu.

Ameongeza kuwa ili kuvutia wawekezaji wa nje, ni muhimu kuwa na wananchi walioboreshwa kitaaluma na kiutendaji katika sekta ya huduma. Amesema katika hafla hiyo ya tuzo, imeonekana wazi kuwa watanzania wengi sasa ndio wanaosimamia huduma, kukutana na wateja, na kuendesha shughuli kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Dkt. Serera ametahadharisha kuwa taasisi au kampuni yoyote isiyotoa huduma bora inahatarisha kupoteza wateja wake, akisema, “Mteja akihudumiwa vibaya, ni rahisi asirudi tena. Hivyo, huduma bora ni msingi wa biashara endelevu.

Kadhalila, Dkt. Serera amehimiza taasisi zote, hususan za serikali, kuendelea kuboresha huduma zao, akisema hata wale ambao hawajapata tuzo mwaka huu wamepata fursa ya kujifunza na kuboresha zaidi huduma wanazozitoa kwa wananchi.

Aidha, ameipongeza taasisi ya CSW kwa kuandaa hafla hiyo ambayo ilihusisha utoaji wa zaidi ya tuzo 20 kwa taasisi na kampuni zilizoonyesha ubora wa huduma katika Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji wa CSW Group Bi Annelise Nyangusi amesema kuwa katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, huduma kwa wateja ni chachu muhimu ya kukuza biashara na kampuni hivyo kama CSW Tanzania, wameona umuhimu wa kutambua na kutunuku kampuni, mashirika na wafanyabiashara wanaofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wateja, kwa kuzingatia vigezo maalum vinavyoonyesha ubora wa utendaji wao.