Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kikao cha rasimu na kukusanya maoni yatakayo boresha sera ya maendeleo ya viwanda ya mwaka 1996-2020 iliyotolewa mwaka 2025, Machi 11, 2025


Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah ameongoza kikao maalum cha Kikundi kazi cha Maendeleo ya viwanda kimekutana na wajumbe pamoja na wadau kwa ajili ya kuchambua rasimu na kukusanya maoni yatakayo boresha sera ya maendeleo ya viwanda ya mwaka 1996-2020 iliyotolewa mwaka 2025, Machi 11, 2025 jijini Dar Es Salaam.

Baadhi ya maoni ambayo yamepokelewa kwenye kikao hicho ni pamoja na masuala ya umeme, malighafi, teknolojia, kodi na rasilimali watu.

Dkt. Abdallah amesema kuwa rasimu hiyo imeandaliwa na kikundi kazi maalum, hivyo maoni yao yanakwenda kuweka mazingira wezeshi kwenye uzalishaji.

"Huu ni mkutano ambao umekwenda kutafsiri kwa vitendo ile dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweka mazingira wezeshi kwenye uzalishaji viwandani na kwenye biashara,"amesema Dkt. Hashil.

Ameongeza kuwa mkutano huo umekusanya sampuli kubwa na muhimu ambazo zinatumika duniani kwa sekta za umma na binafsi ambao wana maamuzi makubwa.

Aidha. Dkt. Abdallah amewahakikishia wadau wote kuhusu maoni walioyatoa katika kufanya maboresho ya sera ya Maendeleo ya Viwanda wameyachukua na watafanyiakazi kwa kuyachakata ili kuweka misingi ya uchumi yaweze kufanikiwa kwa nyaraka wanazokwenda kuandaa.

Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Lwanga amesema wamepokea maoni kutoka kwa wajumbe na wadau wa uchumi na sekta zote za biashara na wamekubaliana kwa wale wanaoendelea kutoa maoni wapeleke hadi Machi 18, 2025.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni za AmiHamza, Amir Hamza amesema ushirikishwaji wa kutoa maoni utatengeneza mazingira rafiki ya uzalishaji kwani wanatoa maoni kulingana na changamoto zilizopo.

Amesema maoni yanayokusanywa yasiishie kwenye viwanda vya Dar Es Salaam bali yafike hadi mikoani hususani kwenye viwanda vilivyopo jirani na mipaka ya nchi ili kujua changamoto zilizopo katika kuboresha sera za viwanda.

Amir amesema wakifika kwa wawekezaji wa mikoani wanaweza kupewa maoni yenye ubora pia kwa kuwa wapojirani na nchi jirani ambazo wakati mwingine zinahitaji bidhaa kutoka nchini hivyo itasaidia kuweka mazingira safi ya uzalishaji na ufanyaji wa biashara.