Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MKURUGENZI MTENDAJI WA WRRB ATEMBELEA WILAYA YA NYASA NA MBINGA MKOA WA RUVUMA


MKURUGENZI MTENDAJI WA WRRB ATEMBELEA WILAYA YA NYASA NA MBINGA MKOA WA RUVUMA

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, ametembelea Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika eneo hilo.

Akiwa Wilayani Nyasa, Bw. Bangu amekutana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Peres Magiri, ambaye amepongeza namna ambavyo mfumo huo unawanufaisha wadau wake, hususan wakulima, kwa kuwapatia bei shindani kwa mazao yao.

Mhe. Magiri ametoa wito kwa Bodi kuendelea kuhamasisha ujenzi wa maghala ya kisasa ndani ya Wilaya hiyo ili kuwezesha minada ya mazao kufanyika katika eneo hilo badala ya kuyasafirisha kwenda Wilaya nyingine. Ameeleza kuwa hatua hiyo itachochea uzalishaji wa mazao ya Ufuta, Mbaazi, Soya na Kakao, ambayo kwa sasa huzalishwa kwa kiwango kidogo licha ya kuuzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Aidha, Bw. Bangu ametembelea maghala na viwanda vya kukoboa kahawa vya kampuni za DAE Co. Ltd na MCCCO Ltd, vinavyotekeleza mfumo huo kupitia utaratibu wa Meneja Dhamana (Collateral Management) katika Wilaya ya Mbinga, Mkoani Ruvuma.

Katika maeneo hayo, Mkurugenzi Mtendaji amezielekeza kampuni husika kuzingatia sheria na taratibu wakati wa utekelezaji wa shughuli zao, hasa katika masuala ya ubora wa mizigo, upimaji, upangaji, usafi wa maeneo ya kuhifadhi, pamoja na utunzaji wa kumbukumbu.

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha mfumo huu unatekelezwa kwa ufanisi, kwa lengo la kuongeza tija kwa wakulima na kuchangia katika kukuza uchumi wa maeneo ya uzalishaji.