Habari
FCC ONGEZENI NGUVU KATIKA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA NA KUMLINDA MLAJI
FCC ONGEZENI NGUVU KATIKA KUDHIBITI BIDHAA BANDIA NA KUMLINDA MLAJI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Suleiman Serera ameisisitiza Tume ya Ushindani (FCC), kuongeza nguvu katika Udhibiti wa Bidhaa Bandia hususani kipindi hiki ambacho tumeingia katika Eneo Huru la Biashara Afrika (AFCTA) ili kutimiza azma ya Serikali ya kukuza Uchumi.
Dkt. Serera ameyasema hayo Aprili 25, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara yake katika Ofisi za Tume ya Ushindani (FCC) ili kujifunza na kujua shughuli za Taasisi na kuweza kufahamiana na Watendaji wa Tume.
Aidha, Dkt. Suleiman Serera ameitaka FCC kuhakikisha inaongeza nguvu kubwa katika kudhibiti bidhaa zinazoingia nchini kupitia mipaka yote ya Bandari na Nchi Kavu ili kuwalinda walaji na uchumi kwa ujumla.
"Tunapowalinda walaji tunajilinda na sisi ambao tunatumia bidhaa na tunalinda uchumi kwa maana ya kwamba soko la ushindani litakuwa kubwa na lenye tija".
Mbali na hayo amewapongeza watumishi wote wa FCC kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazofanya katika kuwalinda walaji na kuitaka FCC kuendelea kutoa elimu zaidi kwa jamii na wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili waweze kuelewa masuala ya Ushindani, Udhibiti wa Bidhaa Bandia na Kumlinda Mlaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tafiti, Miungano ya Makampuni na Utoaji Elimu Bi. Zaytun Kikula akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa FCC, amemshukuru Dkt. Serera kwa ziara hiyo na ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuendelea kushirikiana na FCC katika utekelezaji wa majukumu yake.