Serikali imejipanga kuhakikisha chakula kinachozalishwa na kuuzwa nchini ni salama kwa afya ya mlaji na kuwa itachukua hatua kali kwa yeyote atakayevuruga usalama wa chakula.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb), Juni 9, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani, amesema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na dharura za usalama wa chakula ili kulinda afya ya wananchi na kuimarisha mifumo ya chakula.
Aidha, Naibu Waziri amezielekeza Halmashauri kushirikiana na taasisi za Kisekta kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa chakula salama na kuwataka wananchi kuwa makini kwa kusoma lebo, kuchunguza ubora wa chakula na kuhakikisha usafi katika maeneo ya maandalizi na uuzaji wa vyakula.
Hatahivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Profesa Othman Chande, amesema TBS itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kila chakula kinachopatikana sokoni ni salama kwa matumizi ya binadamu na kusisitiza kuwa usalama wa chakula ni msingi wa afya ya Taifa na maendeleo ya kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi amesema athari za chakula kisicho salama ni pamoja na kupunguza nguvu kazi ya Taifa kutokana na magonjwa. Ameongeza kuwa TBS kwa kushirikiana na wadau, imeandaa Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na dharura za chakula hatarishi ili kuweka hatua za haraka na kinga endapo litatokea tatizo la usalama wa chakula nchini na kutoa wito kwa jamii kuzingatia Sayansi katika hatua zote za maandalizi ya chakula