Habari
SERIKALI YADHAMIRIA KUBORESHA HUDUMA ZA UMMA KUPITIA KUWAJENGEA UWEZO WATUMISHI

Serikali kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kuwajengea uwezo watumishi wa Umma kwa lengo la kuendelea kuwahudumia vyema wananchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni-BRELA Septemba 19, 2025 jijini Arusha.
Dkt. Abdallah kuwa kikao cha Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha kisheria na ni sehemu muhimu ya ushirikishwaji wa watumishi katika kufanya maamuzi yanayohusu maslahi yao na
maendeleo ya taasisi kwa ujumla. Kupitia kikao hicho, watumishi wanapata fursa ya kujadili kwa uwazi na kwa pamoja changamoto zinazowakabili wafanyakazi, mafanikio yaliyopatikana, na mikakati ya kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku, hasa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, amempongeza kwa dhati Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, kwa uongozi bora, usimamizi makini na jitihada kubwa za kuhakikisha taasisi inatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mafanikio ambayo BRELA imeyapata katika kipindi cha hivi karibuni yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi wake thabiti, ushirikiano wa karibu na Menejimenti pamoja na mshikamano wa wafanyakazi wote.
Hatahivyo amewahakikishia kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na watumishi bega kwa bega ili kuhakikisha BRELA inaendelea kuwa Chombo imara cha Serikali katika kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza biashara na uwekezaji nchini.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema kuwa lengo la kikao hicho nikupitia na kujadili Taarifa ya Utendaji ya Wakala kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 pamoja na Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Wakala (2021/2022 - 2025/2026) kwa kipindi cha miakaminne (4).
Hii ni hatua muhimu sana, kwakua inatoa fursa ya kutathmini utekelezaji
wa majukumu ya Wakala wa Usajili Wa Biashara na Leseni, kufahamu mafanikio
yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na kuja na mikakati madhubuti ya
kuimarisha zaidi utendaji wake kwa miaka ijayo.