Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI YAENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI


SERIKALI YAENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA WAWEKEZAJI

Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa lengo la kupunguza utegemezi wa bidhaa nje ya nchi, ambapo hadi sasa jumla ya leseni 225 za viwanda na vyeti 29 vya usajili vimetolewa.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameeleza hayo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2025-2026 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma, Aprili 9, 2025.

Aidha Majaliwa amezungumzia jitihada za serikali katika kuhakikisha uzalishaji wa sukari unakidhi mahitaji ya wananchi, akitaja utekelezaji wa mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, kilichozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 7, 2024. Kiwanda hicho, chenye uwezo wa kuzalisha tani 30,000 kwa mwaka, tayari kimeshazalisha tani 19,124 za sukari na kutoa ajira 2,172 rasmi na zaidi ya 8,000 zisizo rasmi.

Pia ameeleza katika mwaka 2025/2026, serikali itaendelea kuhimiza uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vya mazao ya kimkakati, kuboresha mazingira ya biashara, na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi. Aidha, serikali itaendelea kuongeza uwezo wa mifumo ya masoko nchini, ikiwa ni pamoja na mfumo wa stakabadhi za ghala, ili kuboresha ufanisi wa biashara na kutoa fursa za masoko kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.