Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SERIKALI KULINDA MASOKO YA NDANI  ASEMA WAZIRI KAPINGA


📌Afanya ziara kutembelea Viwanda vilivyopo mkoa wa Mbeya;

📌Asema changamoto za wazalishaji kupatiwa ufumbuzi ili kuongeza ufanisi;

📌kuimarika kwa Viwanda vya ndani kutaongeza uzalishaji

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb) amesema Serikali imejipanga kulinda masoko ya ndani na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wazalishaji wa bidhaa nchini zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Amesema hayo mkoani Mbeya wakati wa ziara yake katika Viwanda vitatu ikiwemo Kiwanda cha Saruji cha Mbeya Cement, kiwanda cha magodoro na Kiwanda cha TBL, ambapo alikagua shughuli za uzalishaji, kusikiliza changamoto za wazalishaji na kutambua fursa zilizopo katika sekta ya viwanda.

Kapinga amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji wa ndani, kukuza sekta ya viwanda na kuwezesha wazalishaji wazawa kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara na uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali inaendelea kutambua changamoto zinazojitokeza katika uzalishaji kwa kufanya ziara katika maeneo ya viwanda na kukutana moja kwa moja na wadau, hatua ambayo itaiwezesha kupata taarifa sahihi na kuchukua hatua stahiki.

Aidha amesema mazingira bora kwa wazalishaji ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa nchini, kukuza biashara na kuhakikisha wananchi wanapata fursa zaidi kupitia sekta ya viwanda.

Amesema Serikali pia imejipanga kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, hasa viwanda, kutokana na mchango wake katika ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Amesisitiza kuwa Serikali haitakubali changamoto za wafanyabiashara kubaki bila majibu, hivyo ziara katika maeneo ya uzalishaji zitaendelea kutumika kama sehemu ya kusikiliza kero, kutambua fursa na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Amesema kuimarika kwa viwanda vya ndani kutasaidia kuongeza uzalishaji, fursa za ajira na shughuli nyingine za kiuchumi, huku kukiwa na umuhimu wa kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na ukuaji wa sekta hiyo.