Habari
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo (Mb), ametoa wito kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha wanazalisha tafiti zinazouzika na kuzifanya tafiti na bunifu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo (Mb), ametoa wito kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhakikisha wanazalisha tafiti zinazouzika na kuzifanya tafiti na bunifu kuwa biashara zitakazoingiza kipato.
Amebainisha hayo wakati wa kufunga Warsha kuhusu kubidhaisha kazi za utafiti na ubunifu uliofanyika Machi 28, 2025 jijini Dar es Salaam,
Dkt. Jafo amesema kuwa kupitia tafiti na bunifu, nchi inaweza kubadilika na kufikia maendeleo makubwa, kwani tafiti na ubunifu huwezesha kufanya mambo mengi kwa usahihi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inaboresha mazingira ili Watanzania wanufaike na maendeleo kupitia bunifu zao pamoja na kufanya uwekezaji katika sekta ya elimu ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Aidha Dkt. Jafo amewashauri wabunifu wote kuhakikisha wanasajili bunifu zao kupitia BRELA kwa lengo la kulinda bunifu hizo ili pale zitakapotumiwa na watu wengine wabunifu wapate malipo stahiki na kunufaika.
Aidha, Waziri Jafo ametoa wito kwa wenye viwanda kufungua milango kwa vijana wanaohitaji kujifunza kwa vitendo ili kuongeza maarifa, kubaini changamoto zilizopo na kuona namna ambavyo bunifu zao zinaweza kuleta manufaa kwa maslahi ya taifa.
Pia amesisitiza umuhimu wa kutengeneza bunifu zinazoendana na wakati, akisema kuwa kwa sasa dunia inakwenda katika mwelekeo wa teknolojia ya Sanaa ya Akili (AI), hivyo ni muhimu kuwawezesha vijana kuzalisha bunifu zitakazohusisha teknolojia hiyo.
Vilevile, Dkt. Jafo amesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na sekta za umma kwa lengo la kukuza maendeleo.
Amesema kuwa kwa sasa Tanzania inafanya vizuri katika masoko ya kikanda na kimataifa ikiwemo masoko ya SADC, AGOA, na Soko Huria, hivyo ni muhimu kuongeza juhudi zaidi.