Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

MHE.KATAMBI AITAKA SIDO KUJIPANGA UPYA, KUKUZA MAPINDUZI YA VIWANDA VIDOGO NA KATI


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Patrobas Katambi, amelitaka Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kujipanga upya na kufanya kazi kwa kasi, uwajibikaji na bidii, huku kila mtumishi akiwajibika kuonesha ufanisi katika nafasi yake ya kazi.

Katambi ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Shirika la Maendwleo la Viwanda Vidogo (SIDO) Desemba 19,2015 Jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza umuhimu wa shirika hilo kuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati nchini.

Aidha, Naibu Waziri huyo amesisitiza SIDO kutumia tafiti mpya ili kubaini fursa na mwelekeo wa maendeleo ya viwanda, sambamba na kutumia tafiti za awali kubaini changamoto na maeneo yaliyokosewa ili yasijirudie.

“Tufungue fursa zaidi za utoaji wa mikopo na tuwe wabunifu katika kutambua fursa zilizopo. Kinapofunguliwa kiwanda kikubwa, lazima kiwepo pia cha kati, na pale ambapo kiwanda cha kati kipo, viwanda vidogo vinapaswa kuimarishwa,” ameongeza.

Katambi ameeleza kuwa uchumi wa taifa unategemea kwa kiasi kikubwa mapinduzi ya viwanda vikubwa na vya kati, huku akibainisha kuwa viwanda vidogo na vya kati vimekuwa nguzo muhimu katika utoaji wa ajira na mchango wa maendeleo ya kiuchumi.

“Kipaumbele cha Serikali ni kuandaa na kukuza matajiri wa viwanda wa Kitanzania ili mitaji yao ibaki na kuzunguka ndani ya nchi,” amesema Katambi, akisisitiza kuwa viwanda vidogo na vya kati ni msingi wa mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji, amesema shirika hilo linaendelea kuratibu na kusimamia shughuli zote zinazohusiana na maendeleo ya viwanda vidogo na vya kati nchini.

Ametaja mafanikio ya SIDO katika kipindi cha miaka mitano kuwa ni pamoja na uzalishaji wa mashine na vipuri mbalimbali, kuanzishwa kwa viwanda vipya zaidi ya 2,500, pamoja na kuchangia ongezeko la ajira.

Aidha, SIDO imeendeleza programu ya atamizi wa mawazo bunifu, ambapo mawazo bunifu 32 yameatamiwa, pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali, mbinu za biashara na uchakataji wa bidhaa kwa wajasiriamali nchini.