Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA YAZIDI KUTOA FURSA KWA VIJANA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Judith Kapinga (Mb), amesema uwepo wa masoko ya kimataifa unatoa fursa kubwa kwa vijana kupata ajira kwa kuanzisha biashara za kuuza bidhaa za Tanzania nje ya Nchi.

Aidha amebainisha kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mkakati wa mauzo ya nje wa kitaifa, ambao unalenga kuwashirikisha vijana kikamilifu katika utekelezaji wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 18, 2025 katika Mkutano ulioandaliwa na Idara ya Habari - Maelezo, Kapinga amesema Takwimu za mwaka 2024 zinaonyesha sekta ya viwanda ilichangia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa, ikilinganishwa na 7.0 mwaka 2023 huku Ukuaji wa sekta hiyo uliongezeka kutoka asilimia 4.3 mwaka 2023 hadi 4.8 mwaka 2024, kuonyesha uimara wa sekta.

Amesema kwa upande wa biashara, mchango wake umeongezeka kutoka asilimia 8.4 mwaka 2023 hadi 8.6 mwaka 2024, huku kasi ya ukuaji ikipanda hadi asilimia 4.8.

“Ongezeko hili limetokana na maboresho ya mazingira ya biashara, upanuzi wa viwanda, na juhudi za serikali kufungua masoko mapya ya kikanda na kimataifa.

“Thamani ya bidhaa zilizozalishwa viwandani ilifikia Sh. 26,438.5 bilioni mwaka 2023, ikiongezeka kutoka Sh. 25,034.5 bilioni mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 5.6,” amesema.

Bi Kapinga amesema Serikali inasisitiza umuhimu wa kupata masoko ya uhakika. Kwa Afrika, mauzo ya bidhaa za Tanzania yaliwafikia Dola bilioni 3.94 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 40, yakiwemo mazao kama kahawa, tumbaku, vioo, nafaka, viungo, na nyuzi za mkonge.

Aidha ameongeza kuwa Masoko mapya yamefunguliwa kupitia AfCFTA ikiwemo Nigeria, Morocco, Senegal, Ethiopia, Ghana, Algeria, Djibouti, na Guinea.

“Mauzo kwenye soko la Umoja wa Ulaya yameongezeka kutoka Dola milioni 633.5 mwaka 2023 hadi milioni 686.3 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 7.6, kutokana na bidhaa kama parachichi, kakao, kahawa, tumbaku, na madini.

“Kwa soko la Asia, mauzo yalikuwa Dola bilioni 2.92 mwaka 2023 na bilioni 2.84 mwaka 2024, yakiwemo korosho, mazao ya kunde, parachichi, pamba, karanga, na nyama ya mbuzi,” amesema.