Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Jafo Apongeza Ujenzi wa Metrolojia CBE, Atoa Wito kwa Wanafunzi Kuchangamkia Fani


Jafo Apongeza Ujenzi wa Metrolojia CBE, Atoa Wito kwa Wanafunzi Kuchangamkia Fani

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, ameipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa hatua ya ujenzi wa jengo jipya la Metrolojia na Vipimo, akibainisha kuwa fani hiyo ina soko kubwa la ajira nchini na Afrika Mashariki.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake chuoni humo, Waziri Jafo alisema serikali imewekeza Shilingi bilioni 24 katika ujenzi wa jengo hilo kama sehemu ya mkakati wa kuzalisha wataalamu wa ndani.

“Tunahitaji wataalamu wengi wa ndani kwenye sekta hii. Wanafunzi wachangamkie fursa hii badala ya kuendelea kutegemea wataalamu wa nje,” alisema Jafo.

Akiangalia maendeleo ya ujenzi huo unaofanywa na kampuni ya LI JUN Construction, Waziri aliwataka wakandarasi kuhakikisha ubora wa kazi kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kukamilisha kazi kwa wakati.

Naye Mkuu wa CBE, Profesa Edda Lwoga, alieleza kuwa jengo hilo linaloitwa Metrology Complex litatumika kwa maabara, karakana, na kumbi za mihadhara, na litahudumia zaidi ya wanafunzi 4,000 mara tu litakapokamilika.

Jengo hilo, ambalo ujenzi wake ulianza Mei 2023, linatarajiwa kukamilika awamu ya kwanza mwaka 2026, huku awamu ya pili ikitarajiwa kukamilika mwaka 2029.