Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

JAFO ATOA MAELEKEZO KWA MAAFISA BIASHARA


JAFO ATOA MAELEKEZO KWA MAAFISA BIASHARA

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb) amewataka Maafisa Biashara wa Mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa umakini na ufanisi mfumo wa stakabadhi ghalani ili kurasimisha taratibu za biashara ndani ya mamlaka za serikali.

Amebainisha hayo katika Mkutano wake wa Pili na Maafisa Biashara wa Mikoa uliofanyika mkoani Morogoro Juni 30, 2025 ambapo Dkt. Jafo ameeleza kuwa mfumo huo umeonyesha mafanikio makubwa katika msimu uliopita.

Dkt.Jafo amesema msimu uliopita, kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani mazao yenye thamani ya shilingi trilioni 2.9 yameuzwa ambapo hiyo imesababisha serikali za mitaa kupata mapato ya shilingi bilioni 85 ambapo huo ni ushahidi wa wazi kwamba mfumo huo unaleta tija.

Ameisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani si tu unasaidia wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao, bali pia unarahisisha ukusanyaji wa mapato halali kwa serikali.

Aidha amewaagjza Maafisa hao kusisimamia vizuri mfumo huo, kufanya kazi kwa bidii na kwa pamoja ili kurasimisha biashara, ziwe na tija na mchango mkubwa kwenye pato la taifa.

Vilevile ameeleza kuwa Tanzania inalenga kuwa mzalishaji na msafirishaji na muuzaji mkubwa wa sukari barani Afrika ifikapo mwaka 2027, kufuatia kuongezeka kwa kasi ya uzalishaji wa sukari nchini ambapo nchi imeanza kujiondoa kwenye utegemezi wa sukari kutoka nje.

Amesema hali hiyo inatokana na viwanda vya ndani kuongeza uzalishaji wa sukari kwa kiwango kikubwa nchini kwani kwa sasa mahitaji kwa mwaka ni takribani tani laki 802,000, lakini uzalishaji wa ndani unaendelea kukua kutokana na uwekezaji unaoendelea katika sekta ya viwanda.