Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KAPINGA: UWEZESHAJI WA WANAWAKE NI NGUZO YA MAENDELEO YA UCHUMI


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga(Mb), amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Wanawake Wajasiliamali katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira, kupunguza umaskini na kuimarisha ustawi wa jamii.

Kapinga ameyasema hayo Desemba 19, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 ya Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) na kufungua kikao kazi cha wadau cha kuhakiki taarifa ya awali ya utafiti kuhusu ujumuishaji wa kifedha kidigitali kwa wanawake na vijana wafanyabiashara.

Amesema uwezeshaji wa wanawake kiuchumi una manufaa mapana kwa familia, jamii na Taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wanawake na vijana wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

“Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara, kupanua upatikanaji wa mikopo na huduma jumuishi za kifedha, kukuza ujasiriamali, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kidigitali,” amesema Kapinga.

Aidha Kapinga pia amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na TWCC katika ajenda ya uwezeshaji wa wanawake, hususan katika ujumuishaji wa kifedha kidigitali unaoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa unaoongozwa na teknolojia.

Akizungumzia miaka 20 ya TWCC, Kapinga amesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kuweka dira mpya ya kuwawezesha wanawake kupanua biashara zao hadi masoko ya kikanda na kimataifa, huku wakizingatia biashara za kidigitali na rafiki kwa mazingira.

Amewataka wadau wote, ikiwemo taasisi za kifedha na sekta binafsi, kuimarisha ushirikiano na TWCC katika kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali.

Kwa kaulimbiu ya “Miaka 20 ya kuwezesha wanawake kiuchumi,” Waziri Kapinga alizindua rasmi maadhimisho ya TWCC na kufungua kikao kazi hicho cha wadau.