Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

KATAMBI: MSIWE KIKWAZO KWA WAFANYABIASHARA


Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Patrobas Katambi (Mb), amewataka watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuhakikisha wanatoa huduma zenye matokeo ili kuwasaidia Watanzania kurasimisha biashara zao, huku utoaji wa leseni usiwe kikwazo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Ameyasema hayo Disemba 18, 2025 wakati wa ziara yake katika ofisi za BRELA, akisisitiza kuwa mwekezaji anayekidhi matakwa ya kisheria anapaswa kupewa ushauri sahihi na wa haraka kuhusu hatua za kufuata, badala ya kukumbana na urasimu usio wa lazima.

Amesema katika masuala ya usajili wa makampuni na maeneo ya biashara, BRELA inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa umma ili taarifa za huduma zake ziwafikie Watanzania wengi zaidi.

Aidha Katambi ameeleza kuwa kwa sasa mwelekeo wa taifa unaweka mkazo mkubwa kwa vijana, hivyo sekta ya viwanda na biashara lazima iwe nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Ameongeza kuwa uwekezaji wa kibajeti umeelekezwa zaidi katika kuzalisha ajira, na wizara inalenga kuwa kinara wa kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana kupitia viwanda, biashara na matumizi ya teknolojia sahihi.

Aidha, ameitaka BRELA kufanya tathmini ya kina kubaini idadi ya kampuni zilizosajiliwa, zinazofanya kazi na zisizofanya kazi, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, Mkurugenzi wa Miliki na Ubunifu, Bi. Loy Mhando, amesema wakala huo utayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwa kuongeza juhudi katika utekelezaji wake.