Habari
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe akutana na watumishi wa wizara jijini Dodoma.

Katibu Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu ili kuyafikia matarajio ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaotegemea Viwanda ifikapo mwaka 2025. Akizungumza na watumishi hao kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu Prof. Shemdoe alimshukuru Mhe Rais kwa kumuamini na kumteua na kumuona anafaa kuongoza Wizara hiyo, Prof. Shemdoe aliwataka watumishi kumpa ushirikiano wa kutosha katika utendaji wa kazi kama walivyoonesha ushirikiano kwa Katibu Mkuu mstaafu. “Hii ni wizara iliyobeba ajenda ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya nchi yetu kuwa ya viwanda ili kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya watu hivyo tujue sisi tumepewa jukumu kubwa ambalo tunapaswa kufanya ili wizara hii itoe matokeo yanayotarajiwa na Mhe. Rais Magufuli. “Nawahakikishia kuwapa ushirikiano na wakati wote ofisi yangu itakuwa wazi bila kikwazo chochote muda wote nitapatikana nitakapohitajika. Akielezea matarajio yake kwa watumishi hao Prof. Shemdoe aliwataka kusimamia ajenda ya Tanzania ya Viwanda na pia anatarajia kuwa watafanya kazi kwa uharaka na ufanisi. Naye Katibu Mkuu aliyemaliza muda wake Prof. Joseph Buchweishaija alimpongeza Prof. Shemdoe kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hiyo. “Nampongeza Prof. Shemdoe kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hii, hii ni wizara yenye watu wanaojituma na kufanya kazi kuanzia uongozi wa juu hadi wafanyakazi wa chini”. Akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Bw. Ludovick Nduhiye alieleza kuwa lengo la kikao hicho ni kufahamiana na kutambuana na alihaidi kufanyika kwa kikao kingine cha kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji na changamoto za watumishi. Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi (TUGHE) Wizara ya Viwanda alielezea kuhusu umuhimu wa baraza la wafanyakazi katika kupitisha bajeti ya Wizara. “Ulidokeza kuhusiana na maandalizi ya bajeti ya Wizara, Tunatakiwa kupata wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, tunarajia mwezi huu wa pili kamishina wa kazi atakuja kwa ajili ya kufanya uchaguzi ili baade baraza hilo liweze kupitisha bajeti ya Wizara kama ilivyo utaratibu”.