Habari
KIWANDA CHA KUBANGUA KOROSHO TUNDURU KUANZA KAZI MWAKA HUU
Serikali imesema Mwekezaji wa kiwanda cha kubangua korosho kilichopo wilayani Tunduru Sunil Kamath yupo katika hatua za awali za maandalizi ya kufungua kiwanda hicho.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo (Mb), Januari 30, 2026, Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbuge wa Tunduru, Mhe. Ado Shaibu, katika swali lake, Mbunge huyo ametaka kujua ni lini Serikali itatekeleza maagizo ya Rais Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ya kufufua kiwanda cha kubangua korosho wilayani Tunduru.
Akijibu swali hilo, Londo amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na mwekezaji ili kiwanda kirudi katika uzalishaji na kuendelezwa kulingana na mahitaji yaliyopo.
Katika swali la nyongeza Mbunge huyo amehoji kwa kuwa ahadi hiyo imekuwa ya siku nyingi ni kwanini Serikali isivunje mkataba na mwekezaji huyo na kukabidhi kiwanda kwa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU).
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Londo amesema mwekezaji ameshaahidi kukifungua mwaka huu kwa ajili ya kuanza shughuli za uwekezaji.
Kadhalika amesema kuna eneo limetengwa kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kubangulia korosho Tunduru ili kuweka uchumi jumuishi kwa wananchi na kuwawezesha kulimiki mnyororo wa thamani.
