Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Viwanda na Biashara

Habari

Kiliniki ya Biashara kuanza kutolewa soko la Kariakoo


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ( Mb) ameiagiza Wakala wa usajili wa Biashara na  leseni nchini Tanzania  (BRELA) kuanza utaratibu wa kiliniki ya biashara kwa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo ili kila mtu anayefungua biashara hapo atambuliwe katika mfumo rasmi wa kulipa kodi.

Waziri Kijaji ameyasema hayo 11  Mei, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa Kikao na wafanyabiashara  wa Kariakoo, kilichowashirikisha Mawaziri kutoka Sekta ya Biashara,  Uwekezaji, Fedha, Mambo ya ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na   Ofisi ya Rais TAMISEMI .

Dkt kijaji alibainisha kuwa Kikao hicho kililenga kujibu hoja kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao walizowasilisha katika kikao chao na  Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasimu Majaliwa mwaka jana 2023.

Dkt. Kijaji amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa, hoja zote 21 walizowasilishwa kwa Mhe. Waziri Mkuu zimeanza kutatuliwa ambapo hadi sasa, 16 zimefanyiwa kazi na hoja 5 zilizobaki zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo hoja zinazohusu  kodi.  

Aidha, Dkt. Kijaji amewashauri wafanyabiashara kutofunga biashara zao pale wanapohisi kuwa na changamoto, kwani kufunga biashara kunamnyima haki Mwananchi kupata huduma, pia Serikali kukosa mapato ambayo ndiyo chachu ya kuleta Maendeleo kwa wananchi.

 "Niwaombe  wote kulipa kodi kadri inavyostahili sisi Serikali tutatimiza wajibu wetu, nanyi pia kwa upande wenu timizeni wajibu wenu, kuhusu hili nawaagiza BRELA kuanzisha kiliniki ya biashara. Kila mfanyabiashara kuanzia ngazi ya chini,ya kati hadi mkubwa kutambuliwa na kuingizwa kwenye mfumo wa kulipa kodi".Amesema kijaji

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa  Serikali itaendelea kuweka mazingira Bora ya biashara ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji na kukuza   uchumi Mpya

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) alisema Mei 25,2024 watapitia hatua mpya za kikodi na kwamba hoja zote zinazohusu kodi kwa wafanyabiashara zitajadiliwa.