Habari
Kiwanda cha KMTC Manufacturing Limited kilichopo Moshi,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amefanya ziara ya kikazi katika Kiwanda cha KMTC Manufacturing Limited kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro. Kiwanda hicho kinasimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kinajihusisha na uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa maendeleo ya viwanda na uchumi wa Taifa.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia maendeleo ya kiwanda, kuangalia hali ya uzalishaji, changamoto zilizopo, na kujadili mikakati ya kuongeza tija katika mchango wa kiwanda hicho kwa uchumi wa nchi na ajenda ya Serikali ya kukuza viwanda kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, Dkt. Abdallah alitembelea maeneo mbalimbali ya kiwanda ikiwa ni pamoja na eneo la uzalishaji na ghala la kuhifadhia bidhaa. Pia alipokea maelezo kutoka kwa uongozi wa kiwanda kuhusu teknolojia inayotumika, uwezo wa uzalishaji, masoko ya bidhaa, pamoja na mchango wa kiwanda katika kutoa ajira.
Aidha, Dkt. Abdallah alifanya majadiliano na menejimenti ya KMTC pamoja na maofisa kutoka NDC kuhusu fursa zilizopo na changamoto zinazolikabili kiwanda hicho.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Abdallah alisisitiza umuhimu wa kuongeza kiwango cha uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, kuboresha ubora wa bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko ya kimataifa, na kuimarisha ushirikiano kati ya NDC na sekta binafsi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji zaidi kwenye sekta ya viwanda.
Vilevile, aliahidi kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na kuhakikisha changamoto zinazoathiri ufanisi wa kiwanda hicho, zikiwemo upatikanaji wa mitaji na masoko, zinapatiwa ufumbuzi wa haraka.