Tushiriki katika Michezo kuimarisha Afya.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Bahi Bw. Subiri Kajuni akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo amewaasa watumishi wa Serikali na Taasisi kuendelea na utamaduni wa kushiriki katika michezo mbalimbali ili kuimarisha afya zao.
Amebainisha hayo katika Bonanza lililoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara lililofanyika katika viwanja vya Misheni Wilaya ya Bahi Machi 15,2025.
Bw.Kajuni amesema ushiriki wa watumishi katika michezo unasaidia kuboresha afya pia kuondokana na magonjwa yasioambukiza pamoja na kujenga mahusiano mazuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utawala Wizara ya Viwanda na Biashara Bi.Ingrid Sanda amesema kama Wizara imekuwa ikiandaa mabonanza mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kujenga afya pamoja na kujiandaa na Michezo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Mei Mosi pamoja na SHIMIWI.
Aidha amesema kutakuwa na muendelezo wa mabonanza kama hayo katika taasisi mbalimbali ili kufanikisha adhma hiyo pamoja na kujenga mahusiano mazuri baina ya Wizara na taasisi watakazoshirikiana nazo.
Nae Afisa Michezo,Sanaa na Utamaduni wa Wilaya ya Bahi Bi.Rachel Mwitula amesema amefurahishwa na bonanza hilo na kuishukuru Wizara kwa kufanikisha bonanza hilo kwani imepelekea kuanzisha ushirikiano pamoja na kubadilishana uzoefu.