Habari
LONDO: SIMAMIENI KWA UADILIFU UKAGUZI WA VIPIMO
Serikali imewataka watumishi wa Wakala wa Vipimo (WMA) Nchini kusimamia kwa uadilifu ukaguzi wa vipimo na kutokubali udanganyifu unaoweza kuhatarisha ubora wa bidhaa na kudhoofisha imani ya wananchi na wafanyabiashara, huku ikieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dennis Londo(Mb) kwaniaba ya Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Judith Kapinga wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 38 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo(WMA) Agosti 2,2026 Jijini Arusha ambapo amewasihi kutokubali kuchezewa kwa vipimo au viwango kwa maslahi binafsi, akisema jukumu lao ni kulinda ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoingia kutoka nje ili ziweze kushindana katika soko la kikanda na kimataifa.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Wakala wa Vipimo ilifanikiwa kuhakiki vipimo zaidi ya milioni 5.5 nchini, mafanikio ambayo yameongeza ulinzi wa walaji na kuimarisha mazingira ya biashara ambapo ameingeza kuwa WMA imefanya kazi kubwa ya kulinda uchumi wa nchi kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinazingatia viwango vinavyotakiwa.
Alieleza kuwa serikali imeendelea kusogeza huduma za wakala kwa wananchi kwa kuanzisha ofisi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma za uhakiki wa vipimo na kuongeza kuwa biashara haiwezi kukua bila kuwepo kwa imani kati ya mnunuzi na muuzaji, hivyo vipimo sahihi ndiyo msingi wa kujenga imani hiyo, hasa katika kipindi hiki ambacho biashara nyingi zinafanyika kwa njia za kidijitali.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Alban Kihulla ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo amesema ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi umekuwa chachu ya kutatua changamoto mbalimbali.
Pia wakala wa vipimo imezindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31, ambao utakuwa mwongozo wa utekelezaji wa shughuli zote za taasisi katika kipindi hicho kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na unalenga kuimarisha utendaji wa taasisi.
